C6: AFYA YA MENO KUTOKA KWA MTAALAMU (DENTAL HEALTH TIPS FROM A DENTIST) || ZIJUE SABABU ZINAZOPELEKEA HARUFU MBAYA YA KINYWA HATA BAADA YA KUPIGA MSWAKI.

 Na Mwandishi Arnold Lusingo (Mwandishi ni mwanafunzi wa udaktari wa afya ya kinywa katika Chuo cha Primary health care Institute, Iringa Contacts: Twitter@kakadentine, FB: Arnold Lusingo)

Tatizo la kutoa harufu mbaya kwenye kinywa hata baada ya kusafisha kinywa  limewakumba watu wengi sana na wao bila kujua sababu ya harufu hizo wametumia dawa mbalimbali za kienyeji na hata za hospitali bila mafanikio wala mabadiliko yoyote.

 Hata hivyo zipo sababu nyingi zinahusishwa kuwa kama ni sababu kuu kusababisha harufu isiyoisha kutoka kwenye kinywa cha mtu, sababu hizo ni kama ifuatavyo.

1. Usafishaji mbovu wa kinywa (poor oral hygiene)

2. Uwepo wa jino lililotoboka na kuhifadhi mabaki ya vyakula.

3. Uwepo wa uchafu mgumu usioweza kutoka kwa mswaki ugaka (calculus).

4. Magonjwa ya fizi kwa namna zake(gingivitis, periodontitis).

5. Kuwepo kwa nyama iliyofunika jino linaloota hasa meno ya nyuma (flap).

6. Magonjwa mengine ya mifumo ya mwili(other systemic diseases).

7. Unywaji pombe.

Hizo hapo juu ni sababu ambazo zimeonekana mara nyingi kuwa vyanzo vya harufu mbaya kwenye kinywa isiyoisha. Hata hivyo zipo namna zinazoweza kufanyika kuondoa hivyo visababishi vya harufu mbaya kwenye kinywa kutegemeana na kisababishi. 

1. Usafishaji mbovu wa kinywa(poor oral hygiene)

 Usafishaji usiosahihi wa meno huweza kusababishwa na yafuatayo.

Mswaki uliochakaa sana hivyo kushindwa kuondoa mabaki yote ya chakula, njia mbaya kusafisha kinywa(poor brushing technique), baadhi ya sehemu za kinywa hazikufikiwa na mswaki haswa sehemu za nyuma za meno ya nyuma, na pia sehemu za ulimi.

Hii hukingwa kwa kufanya yafuatayo, kubadilisha mswaki mara kwa mara angalu mara moja kwa kila miezi miwili,kuhakikisha kila sehemu ya kinywa imesafishwa vizuri kwa mswaki mzima(ambao haujachakaa). Kusafisha kinywa chako angalau mara mbili kwa siku kila siku asubuhi baada ya kifungua kinywa na usiku kabla ya kulala. Kwa kufanya hayo utakuwa umeweza kuzuia harufu hiyo kwa sehemu fulani. 

2.Uwepo wa jino lililotoboka na kuhifadhi mabaki ya vyakula.

Uwepo wa jino au meno yaliyotoboka kwenye kinywa huweza kusababisha harufu kwenye kinywa chako sababu tundu lililopo kwenye jino huweza kuhifadhi mabaki ya chakula, ambayo wakati wa kusafisha hayawezi kutoka sababu mswaki sio mdogo kiasi cha kuweza kupenya katikati ya tundu hilo na hivyo kupelekea mabaki hayo kuoza na kusababisha harufu isiyoisha.

Njia pekee ya kuweza kuzuia harufu isiyoisha inayosababishwa na uwepo wa jino au meno yaliyoyoboka ni kupata huduma ambayo pekee yake inatolewa kwa usalama zaidi katika hospitali au kliniki zinazotoa huduma za matibabu ya kinywa na meno. Huduma unazoweza kuzipata ukienda huko zinatolewa kutegemeana na kiasi cha uharibifu wa jino, kama jino limetoboka kidogo na haliumi au linauma kidogo jino hilo litasafishwa kwa vifaa maalumu na kuwekewa dawa ya kuliziba ambapo utalitumia jino lako kama kawaida. Lakini kama jino limetoboka sana na linauma pia kuna matibabu ya aina mbili aidha kuuwa mzizi wa jino la kuliziba au kulitoa jino lote.

NB: usisubiri mpaka jino liume sana ndo uende hospitali, ni lazima litatolewa tu, kiafya zaidi unashauriwa kuhudhuria kwaajili ya uchunguzi wa meno ili kabla meno hayajaharibika sana yazibwe mapema. 


Picha hapa juu inaonesha jino liliotoboka likiwa na mabaki ya chakula yaliyoshindwa kutoka kwa mswaki.

3. Uwepo wa uchafu mgumu usioweza kutoka kwa mswaki, ugaka (calculus).

Upo uchafu mgumu ambao hukaa kwenye meno au kwenye nafasi katikati ya fizi na jino(gingival sulcus) ambao hauwezi kutoka kwa mswaki au kwa dawa isipokuwa kwa matibabu ya kuusafisha ambayo hufanyika kwenye kliniki zinazotoa huduma ya kinywa na meno kwa kuusafisha kwa vifaa maalumu kwa huduma inayoitwa kwa jina la kitabibu (scaling and root planning).

Uchafu huu huganda na mabaki ya chakula ambayo yanafanya uchafu ubaki hapo mwisho huoza na kutoa harufu, pia calculus hupelekea magonjwa ya fizi ambayo kwa kitabibu huitwa periodontitis ambayo ni hatari kwa afya ya kinywa. Njia pekee ya kutoa uchafu huu ni kufika kwenye kliniki yoyote inayotoa huduma ya kinywa na meno kwa ajili ya kusafishwa na vifaa maalumu. 

.

Picha hapa juu inaonesha uchafu mgumu kwenye meno ambao hautoki kwa mswaki (calculus/tartar)

 4. Magonjwa ya fizi kwa namna zake (gingivitis, periodontitis).

Magonjwa ya fizi kwa namna zake nayo pia hupelekea kuwepo kwa harufu mbaya kwenye kinywa cha mtu hata baada ya kusafishwa. Mtu mwenye magonjwa ya fizi kama(periodontitis) huwa na sifa zifuatazo kwenye kinywa chake, nafasi kati ya fizi na jino(gingival sulcus) huongezeka na kuwa kama mfuko(gingival pockets) ambazo huhifadhi mabaki ya chakula, na pia ni vigumu kusafisha mabaki ya chakula humo, hivyo, hii pia huweza kusababisha mabaki hayo kuoza na kutoa harufu.

Hii pia huwezi kujitibu wewe mwenyewe au kwa dawa za kung'ata bali utatibiwa na matabibu meno kwa huduma maalumu lakini pia utapewa dawa ambazo zitasidia kurudi katika hali yako ya kiafya na utapewa ushauri nasaha juu ya namna nzuri ya kutunza kinywa chako. Hivo ni heri ukawahi mapema kabla hujapata madhara zaidi kwenye kinywa chako. 


 

Picha hapo juu inaonesha jino lenye afya na jino lililopata magonjwa ya fizi yaan periodontitis.

  5. Kuwepo kwa nyama iliyofunika jino linaloota hasa meno ya nyuma (flap).

Kwa watu wengi, meno ya mwisho ya taya ya chini huwa hayaoti mpaka kuonekana kabisa kwenye kinywa, hii inasababishwa na kuwa na taya dogo kushindwa kupokea meno yote kumi na sita. Hivyo basi, jino huota nakuoneka kidogo na sehemu nyingine ya jino ikiwa imefunikwa na nyama fulani ambayo kitabibu huitwa (Flap). Nyama hii huweza kuingia chakula na kwasababu nafasi ni ndogo chini ya nyama hiyo mswaki hauwezi kuingia kusafisha hayo mabaki ya chakula, ambayo huoza na kusababisha harufu kwenye kinywa. Nyama hii inapaswa kutoka kwasababu iliendelea kukaa hapo haitaishia kusababisha harufu tu, bali, huweza kuvimba na kusababisha maumivu makali sana ambayo yanaweza hata kukukosesha usingizi, kitabibu hali hii inaitwa (pericoronitis). Matibabu yake yanapatikana katika kituo chochote kinachotoa huduma ya afya ya kinywa na meno, na matibabu yake ni kukatwa nyama(flap) hiyo.

Picha hapo juu inaonyesha nyama iliyofunika jino(flap)

 6. Magonjwa mengine ya mifumo ya mwili(other systemic diseases).

Hii haitofautiani sana na magonjwa ya fizi sababu magonjwa yanayozungumziwa hapa hasa ni magonjwa yanayoathiri kinga za mwili kama vile kisukari, ukimwi(HIV) na leukemia na mengine mengi. Magonjwa haya huonekana/hujidhihirisha kwenye kinywa chako kwa magonjwa ya fizi yaan periodontitis. Na ili magonjwa ya  fizi yanayotokea kama matokeo ya magonjwa mengine ya mifumo yapone ni lazima uzingatie matibabu ya magonjwa ya mifumo mingine ya mwili, kwa kufanya hivyo matibabu yanaweza kukamilika na kusaidia hata kuondoa harufu mbaya kwenye kinywa. Cha kufanya hapa ni kuzingatia matibabu ya magonjwa hayo na kufuata ushauri wa kitabibu unaoweza kuupata kwenye kliniki yoyote inayotoa huduma ya afya ya kinywa na meno. 

7. Matumizi ya pombe

Matumizi ya vilevi yaanI pombe huweza kusababisha harufu kwenye kinywa hata baada ya kusafisha kinywa kwa sababu, mtu anapokuwa kanywa pombe, inaingia katika mfumo wa chakula na ikifika tumboni pombe huozeshwa(fermentation) na kupelekea kutengeneza harufu mbaya ambayo hutoka tumboni mpaka kinywani, kwa sababu kuna muunganiko wa moja kwa moja kati ya tumbo na kinywa. Hapa pia hata kama mtu atasafisha kinywa chake vizuri bado harufu itakuwepo sababu harufu hiyo haitoki kinywani bali tumboni. Hii pia unaweza kuizuia kwa kuacha matumizi ya pombe. 

HITIMISHO

Harufu mbaya kwenye kinywa chako sio nzuri kabisa kwasababu huweza kukunyima uhuru wakati ukiwa katika kundi la watu na kuongea nao, na mara nyingi unaweza usijijue kama unatoa harufu kwenye kinywa chako mpaka uone watu hawakai jirani na wewe unapoongea.

Ushauri ni huu, jiwekee mazoea ya kwenda kupata huduma za uchunguzi wa afya yako ya kinywa na meno angalau mara mbili kwa mwaka hii itakusaidia wewe kujua hata shida ambazo zingeweza kukusumbua siku za mbeleni kama zisingefanyiwa matibabu mapema.


Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

C5: NOW YOU KNOW (ABOUT MEDICINE): THE PROPER USES OF CAPSULES

C1. THE CLASS WITHOUT WALLS !