C6: AFYA YA MENO KUTOKA KWA MTAALAMU (DENTAL HEALTH TIPS FROM A DENTIST) || ZIJUE SABABU ZINAZOPELEKEA HARUFU MBAYA YA KINYWA HATA BAADA YA KUPIGA MSWAKI.
Na Mwandishi Arnold Lusingo (Mwandishi ni mwanafunzi wa udaktari wa afya ya kinywa katika Chuo cha Primary health care Institute, Iringa Contacts: Twitter@kakadentine, FB: Arnold Lusingo)
Tatizo la kutoa harufu mbaya kwenye kinywa hata baada ya kusafisha kinywa limewakumba watu wengi sana na wao bila kujua sababu ya harufu hizo wametumia dawa mbalimbali za kienyeji na hata za hospitali bila mafanikio wala mabadiliko yoyote.
Hata hivyo zipo
sababu nyingi zinahusishwa kuwa kama ni sababu kuu kusababisha harufu isiyoisha
kutoka kwenye kinywa cha mtu, sababu hizo ni kama ifuatavyo.
1. Usafishaji mbovu wa kinywa (poor oral hygiene)
2. Uwepo wa jino lililotoboka na kuhifadhi mabaki ya
vyakula.
3. Uwepo wa uchafu mgumu usioweza kutoka kwa mswaki ugaka
(calculus).
4. Magonjwa ya fizi kwa namna zake(gingivitis,
periodontitis).
5. Kuwepo kwa nyama iliyofunika jino linaloota hasa meno ya
nyuma (flap).
6. Magonjwa mengine ya mifumo ya mwili(other systemic
diseases).
7. Unywaji pombe.
Hizo hapo juu ni sababu ambazo zimeonekana mara nyingi kuwa
vyanzo vya harufu mbaya kwenye kinywa isiyoisha. Hata hivyo zipo namna
zinazoweza kufanyika kuondoa hivyo visababishi vya harufu mbaya kwenye kinywa
kutegemeana na kisababishi.
1.
Usafishaji mbovu wa kinywa(poor oral hygiene)
Usafishaji usiosahihi wa meno huweza
kusababishwa na yafuatayo.
Mswaki
uliochakaa sana hivyo kushindwa kuondoa mabaki yote ya chakula, njia mbaya
kusafisha kinywa(poor brushing technique), baadhi ya sehemu za kinywa
hazikufikiwa na mswaki haswa sehemu za nyuma za meno ya nyuma, na pia sehemu za
ulimi.
Hii
hukingwa kwa kufanya yafuatayo, kubadilisha mswaki mara kwa mara angalu mara
moja kwa kila miezi miwili,kuhakikisha kila sehemu ya kinywa imesafishwa vizuri
kwa mswaki mzima(ambao haujachakaa). Kusafisha kinywa chako angalau mara mbili
kwa siku kila siku asubuhi baada ya kifungua kinywa na usiku kabla ya kulala.
Kwa kufanya hayo utakuwa umeweza kuzuia harufu hiyo kwa sehemu fulani.
2.Uwepo wa jino lililotoboka na kuhifadhi
mabaki ya vyakula.
Uwepo
wa jino au meno yaliyotoboka kwenye kinywa huweza kusababisha harufu kwenye
kinywa chako sababu tundu lililopo kwenye jino huweza kuhifadhi mabaki ya
chakula, ambayo wakati wa kusafisha hayawezi kutoka sababu mswaki sio mdogo
kiasi cha kuweza kupenya katikati ya tundu hilo na hivyo kupelekea mabaki hayo
kuoza na kusababisha harufu isiyoisha.
Njia
pekee ya kuweza kuzuia harufu isiyoisha inayosababishwa na uwepo wa jino au
meno yaliyoyoboka ni kupata huduma ambayo pekee yake inatolewa kwa usalama
zaidi katika hospitali au kliniki zinazotoa huduma za matibabu ya kinywa na
meno. Huduma unazoweza kuzipata ukienda huko zinatolewa kutegemeana na kiasi
cha uharibifu wa jino, kama jino limetoboka kidogo na haliumi au linauma kidogo
jino hilo litasafishwa kwa vifaa maalumu na kuwekewa dawa ya kuliziba ambapo
utalitumia jino lako kama kawaida. Lakini kama jino limetoboka sana na linauma
pia kuna matibabu ya aina mbili aidha kuuwa mzizi wa jino la kuliziba au kulitoa
jino lote.
NB:
usisubiri mpaka jino liume sana ndo uende hospitali, ni lazima litatolewa tu,
kiafya zaidi unashauriwa kuhudhuria kwaajili ya uchunguzi wa meno ili kabla
meno hayajaharibika sana yazibwe mapema.
![]() |
| Picha hapa juu inaonesha jino liliotoboka likiwa na mabaki ya chakula yaliyoshindwa kutoka kwa mswaki. |
3. Uwepo wa uchafu mgumu usioweza kutoka kwa mswaki, ugaka (calculus).
Upo uchafu mgumu ambao hukaa kwenye meno au kwenye nafasi katikati ya fizi na jino(gingival sulcus) ambao hauwezi kutoka kwa mswaki au kwa dawa isipokuwa kwa matibabu ya kuusafisha ambayo hufanyika kwenye kliniki zinazotoa huduma ya kinywa na meno kwa kuusafisha kwa vifaa maalumu kwa huduma inayoitwa kwa jina la kitabibu (scaling and root planning).
Uchafu huu huganda na mabaki ya chakula
ambayo yanafanya uchafu ubaki hapo mwisho huoza na kutoa harufu, pia calculus
hupelekea magonjwa ya fizi ambayo kwa kitabibu huitwa periodontitis ambayo ni
hatari kwa afya ya kinywa. Njia pekee ya kutoa uchafu huu ni kufika
kwenye kliniki yoyote inayotoa huduma ya kinywa na meno kwa ajili ya kusafishwa
na vifaa maalumu.
.
Picha hapa juu inaonesha uchafu mgumu kwenye meno ambao hautoki kwa mswaki (calculus/tartar)
Magonjwa ya fizi kwa namna zake nayo pia
hupelekea kuwepo kwa harufu mbaya kwenye kinywa cha mtu hata baada ya
kusafishwa. Mtu mwenye magonjwa ya fizi kama(periodontitis) huwa na sifa
zifuatazo kwenye kinywa chake, nafasi kati ya fizi na jino(gingival sulcus) huongezeka
na kuwa kama mfuko(gingival pockets) ambazo huhifadhi mabaki ya chakula, na pia
ni vigumu kusafisha mabaki ya chakula humo, hivyo, hii pia huweza kusababisha
mabaki hayo kuoza na kutoa harufu.
Hii pia huwezi kujitibu wewe mwenyewe au
kwa dawa za kung'ata bali utatibiwa na matabibu meno kwa huduma maalumu lakini
pia utapewa dawa ambazo zitasidia kurudi katika hali yako ya kiafya na utapewa
ushauri nasaha juu ya namna nzuri ya kutunza kinywa chako. Hivo ni heri ukawahi
mapema kabla hujapata madhara zaidi kwenye kinywa chako.
Picha hapo juu inaonesha jino lenye afya na jino lililopata magonjwa ya fizi yaan periodontitis.
Kwa watu wengi, meno ya mwisho ya taya ya chini huwa hayaoti mpaka kuonekana kabisa kwenye kinywa, hii inasababishwa na kuwa na taya dogo kushindwa kupokea meno yote kumi na sita. Hivyo basi, jino huota nakuoneka kidogo na sehemu nyingine ya jino ikiwa imefunikwa na nyama fulani ambayo kitabibu huitwa (Flap). Nyama hii huweza kuingia chakula na kwasababu nafasi ni ndogo chini ya nyama hiyo mswaki hauwezi kuingia kusafisha hayo mabaki ya chakula, ambayo huoza na kusababisha harufu kwenye kinywa. Nyama hii inapaswa kutoka kwasababu iliendelea kukaa hapo haitaishia kusababisha harufu tu, bali, huweza kuvimba na kusababisha maumivu makali sana ambayo yanaweza hata kukukosesha usingizi, kitabibu hali hii inaitwa (pericoronitis). Matibabu yake yanapatikana katika kituo chochote kinachotoa huduma ya afya ya kinywa na meno, na matibabu yake ni kukatwa nyama(flap) hiyo.

Picha hapo juu inaonyesha nyama iliyofunika jino(flap)
Hii haitofautiani sana na magonjwa ya fizi
sababu magonjwa yanayozungumziwa hapa hasa ni magonjwa yanayoathiri kinga za
mwili kama vile kisukari, ukimwi(HIV) na leukemia na mengine mengi. Magonjwa haya huonekana/hujidhihirisha
kwenye kinywa chako kwa magonjwa ya fizi yaan periodontitis. Na ili magonjwa
ya fizi yanayotokea kama matokeo ya
magonjwa mengine ya mifumo yapone ni lazima uzingatie matibabu ya magonjwa ya
mifumo mingine ya mwili, kwa kufanya hivyo matibabu yanaweza kukamilika na
kusaidia hata kuondoa harufu mbaya kwenye kinywa. Cha kufanya hapa ni kuzingatia matibabu ya
magonjwa hayo na kufuata ushauri wa kitabibu unaoweza kuupata kwenye kliniki
yoyote inayotoa huduma ya afya ya kinywa na meno.
7. Matumizi ya pombe
Matumizi ya vilevi yaanI pombe huweza kusababisha harufu kwenye kinywa
hata baada ya kusafisha kinywa kwa sababu, mtu anapokuwa kanywa pombe, inaingia
katika mfumo wa chakula na ikifika tumboni pombe huozeshwa(fermentation) na
kupelekea kutengeneza harufu mbaya ambayo hutoka tumboni mpaka kinywani, kwa
sababu kuna muunganiko wa moja kwa moja kati ya tumbo na kinywa. Hapa pia hata
kama mtu atasafisha kinywa chake vizuri bado harufu itakuwepo sababu harufu
hiyo haitoki kinywani bali tumboni. Hii pia unaweza kuizuia kwa kuacha matumizi
ya pombe.
HITIMISHO
Harufu mbaya kwenye kinywa chako sio nzuri
kabisa kwasababu huweza kukunyima uhuru wakati ukiwa katika kundi la watu na
kuongea nao, na mara nyingi unaweza usijijue kama unatoa harufu kwenye kinywa
chako mpaka uone watu hawakai jirani na wewe unapoongea.
Ushauri ni huu, jiwekee mazoea ya kwenda
kupata huduma za uchunguzi wa afya yako ya kinywa na meno angalau mara mbili
kwa mwaka hii itakusaidia wewe kujua hata shida ambazo zingeweza kukusumbua
siku za mbeleni kama zisingefanyiwa matibabu mapema.

Thank you Dr
ReplyDeleteThanks Dr. Lusingo
ReplyDeleteKazi Bora kabisaa
ReplyDeleteNice article bro,keep pushing and going
ReplyDeletekeep it up dentineš
ReplyDelete